ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba amefichua siri ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), akisema vilikwamisha mchakato huo ili
baadaye viingize vipengele vyao wakiingia madarakani.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Mkendo Musoma
Mjini jana, Jaji Warioba alisema Katiba mpya imebeba mambo mengi mazuri
kwa Watanzania na kwamba kutofautiana kwake na baadhi ya wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba Dodoma, kulitokana tu na vipengele vichache
ambavyo visingeweza kusitisha mchakato mzima wa Katiba hiyo.
Aliongeza kwamba anashangaa ni kwa vipi vyama hivyo vyenye malengo
tofauti kuhusu Katiba hiyo viunde Umoja kwa maslahi ya wananchi. Alisema
kati ya vyama hivyo, kimoja kinataka kuundwe Serikali ya Mkataba huku
kingine kikitaka Serikali tatu.
Alisema nia ya vyama hivi ilikuwa ni kutaka kukwamisha mchakato wa
Katiba Mpya ili baada ya kushika madaraka viingize vile ambavyo vina
maslahi kwao, ikiwemo ya kuvunja Muungano.
Alisema amezungumza na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukubaliana kuwa
baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, mjadala wa Katiba mpya
uendelee.
Hatua hiyo alisema, imesababishwa na Ilani ya CCM ya 2015-2020,
kujikita katika kuboresha maisha ya Mtanzania katika kuwasaidia
kuanzisha na kuboresha shughuli zao za kujipatia kipato, kuboresha
huduma za jamii na miundombinu na kupambana na ufisadi na kuacha
kuzungumzia Katiba mpya.
Ilani hiyo haikugusia mchakato huo wa Katiba ambao ulipita hatua zote
muhimu mpaka kupata Katiba Pendekezwa, na akibakiza kura ya maoni, huku
Ukawa na baadhi ya wajumbe wa tume hiyo, wakitofautiana na Katiba hiyo
kwa madai ya kutozingatia baadhi ya maoni ya wananchi.
Kupoteza uhalali
Akifafanua namna Ukawa ilivyopoteza uhalali, Jaji Warioba alisema
kwanza katika suala la Muungano, kuna chama chenye msimamo wa kuwa na
Muungano wa Mkataba, ambao alisema msimamo huo anaujua ni wa kuvunja
Muungano.
Pili, alisema suala kubwa lililowasumbua wakati wa mchakato wa
kutengeneza Rasimu ya Katiba, ni maadili na kufafanua kuwa Ukawa
iliyojinasibu kutaka kutetea maadili, leo hii ghafla haiwezi tena hata
kuzungumzia rushwa, ndio maana ameona wamejipotezea uhalali wa kutetea
misingi ya maoni ya wananchi.
Uadilifu wa Magufuli
Kwa mujibu wa Warioba, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa
CCM, alikuwa na wasiwasi kama angepatikana mwenye maadili, lakini
alipopatikana Dk John Magufuli, wasiwasi uliondoka kwa kuwa hana
makundi, ameweza kuwaunganisha na ni muadilifu.
Akizungumzia uadilifu wa Dk Magufuli, Jaji Warioba alisema mwaka
1996, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuongoza Tume ya Kero ya Rushwa
ambapo walipofanya uchunguzi, walibaini katika ripoti yao wakaeleza kuwa
rushwa kubwa na nyingi ipo katika ujenzi wa barabara.
Jaji Warioba alisema baada ya Dk Magufuli kuanza kusimamia Wizara ya
Ujenzi, sasa ni miaka 15 hajasikia tena kelele za rushwa katika sekta
hiyo, jambo lililomthibitishia kuwa mgombea huyo ni muadilifu.
Jaji Warioba akifafanua zaidi, alisema ameshangazwa kusikia baadhi ya
makada wa Ukawa, wakiwemo waliowahi kuwa mawaziri wakuu, kusema kuwa
katika miaka 54, Serikali haijafanya jambo lolote.
Alisema alipoingia sekondari, Shule ilikuwa ya Bwiru ikihudumia mikoa
mitano, wakati leo kila kata ina shule moja ya sekondari na wakati huo
hakukua na chuo kikuu lakini leo viko vingi. Kuhusu afya, alisema
Tanzania ya leo hospitali zinafanya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Bugando, matibabu ambayo
yalikuwa yakifanyika nje ya nchi tu.
Alisema hata Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, imeitaka Serikali
kununua mashine ya upasuaji wa kichwa, ambayo haipo na kuhoji hayo si
mafanikio? Katika sekta ya maji, Jaji Warioba alisema maji yamevutwa
kutoka Ziwa Victoria mpaka Shinyanga na sasa yanatarajiwa kwenda Nzega
mpaka Tabora, na kuendelea kuhoji hayo si maendeleo?
Alikwenda mbali zaidi na kuhoji amani ya miaka 54 si maendeleo na
kutaka wnaopinga hilo, waeleze ni nchi gani iliyokaa kwa miaka 54 na
amani kati ya nchi zinazoizunguka Tanzania.
Wanaokana maendeleo
Jaji Warioba alisema anachoshangaa ni baadhi ya watu waliosimamia
maendeleo hayo walipokuwa mawaziri wakuu, kudai kuwa hakuna
kilichofanyika katika miaka 54, wakati walitoa taarifa ya mafanikio ya
utendaji wao ya kila mwaka na kurekodiwa bungeni.
Alisema viongozi hao waliohama CCM na kuingia Ukawa, wamekuwa wakisema uongo na kukana hata mafanikio waliyosimamia wenyewe.
Naye Joseph Lugendo anaripoti kuwa Magufuli, akihutubia umati katika
eneo la Nyamongo mkoani Mara jana kwenye mgodi wa dhahabu wa North Mara
alisema katika maeneo yenye migodi na ujumbe wa kuweka hesabu sawa, kila
kinachochimbwa kijulikane na faida ya mwekezaji na kinachobakia viwe
wazi.
Alisema anawapenda wawekezaji na anawakaribisha waje kuwekeza ili
kutoa ajira, lakini akasema hawaji kutoa zawadi bali kufanya biashara.
Huku akitumia mfano wa mwenye duka na muuzaji, Dk Magufuli amesema
mwenye duka lazima ajue bidhaa zake, mapato yake na faida inayopatikana,
la sivyo atajikuta duka jeupe.
“Hii migodi tumepewa na Mungu, ndio maana hawa wamekuja… hawajaja
kutupa zawadi wamekuja kufanya biashara sasa tutataka hesabu tujue kila
kitu kinachotoka mgodini,” alisema.
Kuhusu watumishi wa umma, Dk Magufuli alisema Serikali atakayoiongoza
itajali kazi zaidi na hivyo mtumishi wa umma atakayeharibu kazi, hakuna
kuhamishwa, ataondoka moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment