MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuwatahadharisha
wananchi kuwa mvua kubwa za el-Nino zinatarajiwa kunyesha kuanzia wiki
ya mwisho ya Septemba, mwaka huu na mwanzoni mwa mwezi Oktoba kama
ilivyokuwa imetabiriwa kutokana na mifumo ya hali ya hewa kuzidi
kuonesha hali hiyo.
Imeeleza kuwa mvua ndogo ndogo zinazoendelea kunyesha maeneo
mbalimbali nchini, ikiwemo jiji la Dar es Salaam si mvua hizo za msimu
wa vuli yaani Oktoba hadi Desemba mwaka huu, ila ni mabadiliko ya hali
ya hewa katika eneo la bahari.
Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi alisema hayo jana wakati akitoa mrejeo wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa.
Alisema mvua za el-Nino bado zipo na kutoa msisitizo kuwa inatarajia
kwa kiasi kikubwa kuchangia mwenendo wa mvua nchini katika kipindi
hicho, kwani hali ya joto mashariki mwa bahari ya Pasifiki inaonesha
kuwepo kwa hali ya el-Nino.
Alisema joto lipo zaidi ya nyuzi joto 2.5 juu ya wastani na
linatarajia kuendelea kuongezeka kufikia nyuzi joto 3.0 kuelekea mwezi
Novemba mwaka huu.
Dk Kijazi alisema pia magharibi mwa bahari ya Hindi hali ya joto ipo
juu ya wastani na inatarajiwa kuendelea kuwa juu ya wastani kiasi cha
nyuzi joto zaidi ya 2.0 kufikia mwezi Novemba mwaka huu wakati mashariki
mwa bahari, joto zaidi chini ya wastani kufikia nyuzi joto -1.5.
“Pamoja na viashiria vingine vya hali ya hewa vinatarajia kusababisha
mvua nyingi hususan katika maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi ambayo
hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka,” alisema.
Hivyo alitaka mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari zinazotakiwa
ili kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo
kubwa zinazotarajia kuanza kunyesha hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment